KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA, MWALIMU J. K. NYERERE, EDINBURGH, SCOTLAND
|
| Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Kamillius Membe |
Ubalozi, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland na Jumuiya ya Watanzania Scotland (TZECA), waliandaa sherehe rasmi ya kumuenzi Baba wa Taaifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, iliyohusisha shughuli mbalimbali zilizofanyika kati ya tarehe 9 na 11 Novemba 2009.
Shughuli zilizofanyika katika sherehe hiyo ni pamoja na Mkutano wa watu mbalimbali maarufu katika chuo hicho kuzungumzia mchango wa Mwalimu katika maendeleo ya Tanzania na ukombozi wa kusini mwa Afrika, uzinduzi wa Nyerere Scholarship kwa ajili ya watanzania kusoma chuoni hapo, na uzinduzi wa Chapisho rasmi la kukumbuka maisha ya Mwalimu, lililoandaliwa na Ubalozi na kuchapishwa na Kampuni ya FIRST ya London.
Mwalimu alisoma Shahada yake ya Pili katika Chuo Kikuu cha Edinburgh na ndio maana Chuo hicho, katika kusherehekea Kumbukumbu ya Miaka 10 toka kifo chake (1999-2009) wakatoa Scholarship mbili kwa ajili ya vijana wa kitanzania na kuandaa shughuli hiyo kwa kumuenzi Mwalimu.
Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili alikuwa Mgeni Rasmi katika sherehe hiyo. Aidha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Benard K. Membe alimwakilisha Mheshimiwa Rais Jakaya M. Kikwete katika sherehe hiyo.
Kauli Mbiu ya shughuli hiyo ilikuwa ni Kuenzi Maisha ya Mwalimu Nyerere (Celebration of the Life of Julius Nyerere). Hii iliangalia maisha ya Mwalimu toka utoto akiwa Butiama mpaka wakati akiwa mwanafunzi na baadae kiongozi wa kitaifa na hatimaye kiongozi wa vita vya ukombozi wa Afrika.
Katika kongamano hilo fupi la kumuenzi Mwalimu wazungumzaji mbalimbali walitoa mada ikiwa ni pamoja na Mzee Mwinyi, Mheshimiwa Membe, Mzee Joseph Butiku (Msaidizi wa karibu wa muda mrefu wa Mwalimu) na wakufunzi pamoja na watafiti mbalimbali wa Chuo Kikuu hicho.
Wengine walioalikwa, lakini wakashindwa kufika kwa kuwa na udhuru mbalimbali, ila wakatuma salamu zao ni pamoja na Rais wa Zamani wa Zambia, Mzee Keneth Kaunda, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Bw. Thabo Mbeki na Mtoto wa Mwalimu, Ndugu Madaraka Nyerere. Mzee Kaunda alituma mwakilishi, Bw. Chipakupaku, aliyewahi kuwa msaidizi wake wa karibu wakati akiwa Rais.
Tamasha hilo lilifanyika katika ukumbi wa chuo kikuu hicho lilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Idada ya Ulaya na Amerika, Balozi Radhia Naima Mtengeti Msuya na Mkuu wa Dawati la Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Bertha Some. Baadhi ya Maafisa wa Ubalozi pia walihudhuria shughuli hiyo, wakiongozwa na Mheshimiwa Balozi Mwanaidi Sinare Maajar. Shirika la Habari la BBC nalo lilituma wawakilishi kwa ajili ya kutoa habari ya shughuli hiyo kwa ajili ya wasikilizaji wa nyumbani.
Katika kongamano hilo, mzungumzaji Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Edinburgh, Dk. Thomas Molony alitoa mada kumuelezea Mwalimu kama msomi mwenye bidii aliyekuwa na mwamko wa kisiasa kusaidia nchi yake. Alisema Mwalimu alionyesha uwezo mkubwa wa kufanya kazi na dalili nzuri ya uongozi alipokuwa chuoni hapo kama mwanafunzi.
Aidha Mheshimiwa Waziri Membe alipewa heshima ya kuzindua sanamu ya kumbukumbu ya Mwalimu chuoni hapo. Katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Waziri alitoa shukrani kwa chuo hicho kwa kumuenzi Mwalimu kwa kutoa scholarships na kuandaa kongamano hilo. Alisema kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kumuenzi Mwalimu kwa kuendeleza aliyoyapigania. Mwishoni Balozi Maajar alitoa shukrani za jumla kwa washiriki wote kwa kupata muda wa kutafakari maisha ya Baba wa Taifa.
Chapisho maalum la kukumbuka miaka 10 toka kufariki dunia kwa Baba wa Taifa lililozinduliwa pia katika sherehe hiyo na Mheshimiwa Waziri Membe lina jumla ya kurasa 66 na kichwa cha habari: “Julius Kambarage Nyerere: Life Times Legacy.” Kampuni ya FIRST, iliyotoa chapisho hilo ni maarufu kwa uchapishaji wake wa Jarida la FIRST Magazine, inayosomwa kila baada ya miezi mitatu kwenye vyumba vya Daraja la Kwanza vya mashirika maarufu ya ndege duniani, kama vile British Airways, United Airline, American Airline, Continental Airline, Air Canada, South African Airways, Etihad, Gulf na Qatar Airways. Chapisho hili limetolewa pia kwenye jarida la mwezi Januari 2010, kama sehemu ya jarida hilo.
Jumla ya waandishi 28, walichangia kwa kutoa makala zilizochapishwa kwenye chapisho hilo. Waandishi hao ni pamoja na watu maarufu kama vile marais wastaafu, Mheshimiwa Benjamin W. Mkapa, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mheshimiwa Joaquim A. Chisano wa Msumbiji. Wengine ni Mawaziri Wakuu Wastaafu Mzee Rashid Mfaume Kawawa, Dk. Salim Ahmed Salim na Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba. Wengine waliochangia ni pamoja na Jaji Mark Bomani, Brigedia Mstaafu Hashim Mbita, Mama Maria Kamm, Prof. Yohana P. Msanjila, Dk. Thomas Molony, Mheshimiwa Pius Msekwa, Bw. Robin White (Mtangazaji Maarufu wa zamani wa BBC Focus on Africa), Balozi Nicholas Kuhanga na Prof. Issa Shivji. Wote walimuelezea Mwalimu kama walivyomfahamu kuwa Kiongozi, mpigania haki za wanyonge duniani, muasisi wa taifa la Tanzania, kwa kuonyesha mafanikio na changamoto mbalimbali wakati wa maisha yake.
Wafanyabiashara mbalimbali walichangia gharama za uchapishaji kwa kutoa matangazo yao ya biashara kwenye chapisho hilo. Wafadhili hao ni pamoja na Ngorongoro Conservation, TANAPA, Anglogold Ashanti, Petrodel, Pan African Energy, Helio Resources, IMMMA Advocates, REXATTORNEYS, PPF, NSSF, TCRA, Serengeti Breweries, Tanzania Trade Center na hoteli za Movenpick, Kempinski na Southern Sun. Pamoja na kulipia matangazo, wote walitoa ujumbe mbalimbali wa kuunga mkono juhudi za kumuenzi Mwalimu.
Ubalozi tayari umeshapokea barua kutoka kwa watu mbalimbali maarufu kama vile, Lord Howe (Waziri wa mambo ya Nje wa Zamani wa Uingereza, Sir Geofrey Howe) wakisifia chapisho hilo na mchango wa Mwalimu katika nchi yetu na Afrika kwa ujumla.
Picha zaidi zinapatikana hapa>>>>>>





